KISWAHILI NEWS: KUKAMATWA KWA WAANDISHI WA HABARI NCHINI TANZANIA

Mamlaka ya Uhamiaji nchini Tanzania imekiri kuwashikilia na baadae kuwaachia huru Waandishi wa Habari wa Kigeni kutoka Kamati ya kutetea haki za Waandishi wa habari yenye makao yake makuu New York Marekani kwa kosa la kufanya jaribio la mkutano wa wandishi wa Habari kinyume na maelezo yao waliyotoa wakati wakiingia nchini humo.
Msemaji wa mamlaka ya uhamiaji nchini Tanzania Ally Mtanda , amemweleza Mwandishi wetu mjini Dar es Salaam kuwa Waandishi hao waliingia mjini Dar es Salaam kama wageni wanaofanya matembezi,lakini baadae wakaanza kuratibu kufanya shughuli za Kiuandishi wa Habari kinyume na sheria na kanuni za uhamiaji kwa mgeni anayeingia nchini kwa matembezi.

Mapema hii leo taarifa za kukamatwa kwa waandishi hao wa habari wa taasisi ya kamati ya kutetea haki za Waandishi wa Habari CPJ ilienea katika mitandao mbaliambali ya kijamii,huku habari hizo zikitofautiana kutoka kwa mtumaji mmoja kwenda kwa mwingine kupitia mitandao ya Whats up na Instagram jijini Dar es Salaam na nje ya mipaka ya Tanzania.
Waandishi hao wa Habari Muthoki Mumo raia wa Kenya na Angela Quintal wa Afrika kusini walishikiliwa jana kwa mahojiano na baadae kuachiliwa mapema leo na kurejea hotelini walipofikia huku hati zao za kusafiria zikiendelea kuwa mikononi mwa maafisa wa uhamiaji kwa uchunguzi zaidi. Msemaji wa Idara ya uhamiaji ya Tanzania Ally Mtanda anaeleza sababu za kushikiliwa na baadae kuachiliwa huru kwa waandishi hao wa Habari..
Nimemuuliza msemaji huyo wa mamlaka ya uhamiaji nchini endapo waandishi hao wangekuwa na athari yoyote kama wangeendelea na mpango wao wa kufanya shughuli za uandishi wa Habari au mikutano na waandishi wengine wa habari hapa nchini...
Mapema Chama cha wahariri wa habari nchini Kenya kilitoa taarifa za kulaani kitendo cha kukamatwa kwa waandishi hao wa habari na kutoa wito kwa serikali ya Tanzania kuwaruhusu kukamilisha kazi yao, ingawa msemaji wa Idara ya uhamiaji Tanzania anasema kuwa kosa la waandishi hao ni kutokujieleza toka wakiingia nchini.